John 13:21-30

Yesu Anatabiri Kusalitiwa Kwake

(Mathayo 26:20-25; Marko 14:17-21; Luka 22:21-23)

21 aBaada ya kusema haya, Yesu alifadhaika sana moyoni, akasema, “Amin, amin nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.”

22Wanafunzi wake wakatazamana bila kujua kuwa alikuwa anamsema nani. 23 bMmoja wa wanafunzi wake ambaye Yesu alimpenda sana, alikuwa ameegama kifuani mwa Yesu. 24Simoni Petro akampungia mkono yule mwanafunzi, akamwambia, “Muulize anamaanisha nani.”

25 cYule mwanafunzi akamwegemea Yesu, akamuuliza, “Bwana, tuambie, ni nani?”

26 dYesu akajibu, “Ni yule nitakayempa hiki kipande cha mkate baada ya kukichovya kwenye bakuli.” Hivyo baada ya kukichovya kile kipande cha mkate, akampa Yuda Iskariote, mwana wa Simoni. 27 eMara tu baada ya kukipokea kile kipande cha mkate, Shetani akamwingia.

Yesu akamwambia Yuda, “Lile unalotaka kulitenda litende haraka.”
28Hakuna hata mmoja wa wale waliokuwa wameketi naye mezani aliyeelewa kwa nini Yesu alimwambia hivyo. 29 fKwa kuwa Yuda alikuwa mtunza fedha, wengine walifikiri Yesu alikuwa amemwambia akanunue vitu vilivyohitajika kwa ajili ya Sikukuu, au kuwapa maskini chochote. 30 gMara tu baada ya kupokea ule mkate, Yuda akatoka nje. Wakati huo ulikuwa ni usiku.

Copyright information for SwhNEN